Na Lucy Ngowi
Dar es Salaam;: WANAFUNZI kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameibuka na uvumbuzi wa kipekee wa mafuta ya nywele na ngozi, wakitumia mabaki ya zabibu yaliyokuwa yakitupwa baada ya matumizi ya awali ya matunda hayo.

Hayo yamebainika katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea mkoani Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, ambapo wanafunzi hao ni miongoni mwa washiriki wakionesha bidhaa zao za ubunifu.
Akizungumza kwa niaba ya chuo hicho, Mwakilishi wa UDOM, Uswege Mwangoge amesema mradi huo ulianzishwa baada ya wanafunzi kubaini kuwa mabaki ya zabibu yanatupwa hovyo, hivyo kuchafua mazingir hali iliwachochea kufikiri na kutafuta namna ya kuyatumia mabaki hayo kwa njia endelevu.
“Tuliona ni upotevu mkubwa kuacha mabaki haya yapotee bure au kuchafua mazingira. Tukafanya utafiti na kugundua kuwa yana virutubisho vingi muhimu kwa ngozi na nywele,” amesema Mwangoge.
Kwa mujibu wa Mwangoge, mafuta hayo yana sifa nyingi za kiafya, ikiwemo uwezo wa kupenya haraka kwenye ngozi, kulainisha, kulinda na kusaidia ngozi kurejea katika hali yake ya asili bila kutumia kemikali hatarishi.
“Mafuta haya yana vitamini nyingi, hayana kemikali, hayachomi ngozi wala kusababisha madhara. Yanasaidia kulainisha ngozi, kuimarisha vinyweleo na kutoa kinga ya asili dhidi ya uharibifu wa ngozi,” amesema.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za UDOM kuhimiza ubunifu, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia bunifu kwa ajili ya maendeleo endelevu na kukuza uchumi wa viwanda kupitia tafiti za wanafunzi.
Kwa sasa, wanafunzi hao wapo katika hatua ya majaribio ya soko huku wakitafuta wadau na wawekezaji watakaosaidia kuongeza uzalishaji na kufikisha bidhaa hiyo sokoni kwa wingi.