Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM – Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, amewatunuku wahitimu 571 waliohitimu mafunzo mbalimbali huku akimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza na kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini pamoja na kuboresha mafunzo ndani ya Jeshi la Polisi, hali iliyoongeza ufanisi wa utendaji wa jeshi hilo.
IGP Wambura amesema hayo wakati akitunuku stashahada na astashahada kwa wahitimu wa fani mbalimbali katika mahafali ya 10 ya vyuo vya taaluma ya Polisi yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA).

Amesema kupitia uongozi wa Rais Samia, Jeshi la Polisi limepatiwa bajeti ya ununuzi wa vifaa vipya na vya kisasa, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na maboresho ya mazingira ya kazi, hatua zinazolenga kuimarisha utendaji wa Jeshi la Polisi kwa viwango vya juu zaidi.
Jumla ya wanafunzi 571 walihitimu kutoka vyuo mbalimbali vya Polisi ambavyo ni Polisi Kidatu, Shule ya Polisi Moshi, Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), Chuo cha Polisi Zanzibar pamoja na Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza.

Wahitimu hao walipata mafunzo katika fani mbalimbali zikiwemo Stashahada ya Sayansi ya Polisi, Shahada ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Astashahada ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Stashahada ya Sayansi ya Tiba ya Maabara, Astashahada ya Ujuzi wa Usalama Majini pamoja na Ujuzi wa Mawasiliano ya Polisi.
IGP Wambura amewapongeza wahitimu kwa kuamua kujiendeleza kielimu, akisema hatua hiyo haina manufaa kwa Jeshi la Polisi pekee bali pia kwa taifa kwa ujumla. Alisisitiza kuwa elimu ni nyenzo muhimu katika kujenga maadili, weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.

“Kuna msemo usemao elimu bora hujenga taifa bora. Elimu ni mwanga unaomwezesha mwanadamu kutambua mema na mabaya,” amesema IGP Wambura huku akinukuu Mithali 4:13 inayosema “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake maana yeye ni uzima wako.”
Ameongeza kuwa elimu na mafunzo waliyoyapata wahitimu hao ni hazina isiyo na kipimo itakayowasaidia katika maisha yao ya kitaaluma, kijamii na kiutumishi.

Aidha, amewataka wakuu wa vyuo vya Polisi kuendelea kuimarisha ushirikiano kupitia mikataba ya makubaliano (MoU) kati ya Jeshi la Polisi na taasisi za elimu ya juu kwa lengo la kuboresha elimu, tafiti na utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kubadilishana wahadhiri, kusaidiana vifaa vya kujifunzia, kupata fursa za ufadhili, kuimarisha mitandao ya kitaaluma pamoja na kuinua hadhi ya vyuo vya Polisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mjumbe wa Bodi ya Ushauri na Mafunzo ya Jeshi la Polisi, Profesa Florence Luoga, amewapongeza wahitimu hao akisema kuhitimu katika vyuo vya Polisi ni ishara ya utayari wa kupokea na kutekeleza majukumu mapya kwa weledi na ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Profesa Luoga amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuongeza uwezo wa kitaaluma katika vyuo vyake kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi na taaluma zitakazowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

