Na Lucy Ngowi
DODOMA: Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Vallensi Wambali amesema vyama vya wafanyakazi ni mhimili muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Pia amesisitiza umuhimu wa uongozi bora, katiba shirikishi, na ushirikiano thabiti kati ya vyama, serikali na waajiri.
Amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake jijini Dodoma.
Amesema ofisi yake inaratibu shughuli zote kuanzia usajili wa vyama, usimamizi hadi hatua ya mwisho kama chama kinataka kujitoa au kushindwa kutimiza masharti ya kisheria.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2019, kifungu cha 43 kinampa mamlaka Msajili wa Vyama kutekeleza majukumu haya,” amesema.
Pia amesema vyama vya wafanyakazi ni kiungo muhimu kati ya wafanyakazi na waajiri katika kuhakikisha kuwepo kwa mahusiano mazuri, uzalishaji wenye tija, na mazingira bora ya kazi.
“Huwezi kuzungumzia uchumi bila nguvu kazi, na huwezi kuzungumzia nguvu kazi bila kuzungumzia wanachama wa vyama vya wafanyakazi. Wanachama ndio uti wa mgongo wa taifa,” amesema Wambali.
Kwa mujibu wa Wambali, ili chama cha wafanyakazi kiwe imara, ni lazima kiwe na uongozi wenye dira, maono na uwezo wa kuwahudumia wanachama wake kwa mujibu wa katiba.
Amebainisha kuwa sheria inaruhusu watu wasiopungua 20 kuanzisha chama, lakini mara tu kinapoanzishwa, lazima kiwe na katiba inayoandaliwa kwa kushirikisha wanachama siyo viongozi peke yao.

“Katiba inapaswa kuakisi matarajio ya wanachama. Inapotungwa na viongozi bila ushirikiano, inakosa uhalali na kuibua migogoro isiyo ya lazima,” ameonya.
Aidha, amehimiza kwamba pamoja na katiba, chama kinapaswa kuwa na kanuni zinazoelezea utekelezaji wake.
“Endapo katiba na kanuni havilingani, huibua changamoto kubwa katika uendeshaji wa chama,” amesema.
Msajili amegusia changamoto zinazotokana na uchaguzi wa viongozi bila kufanya uchunguzi wa kina, kwamba baadhi ya vyama hujikuta na viongozi wasiokuwa na sifa au hata raia wa nchi nyingine, jambo ambalo linaathiri utendaji na kuibua migogoro.
“Ni muhimu kuzingatia mchakato wa uchunguzi wa wagombea ili kuhakikisha kuwa wana sifa stahiki za kuongoza,” amesema.
Wambali amesisitiza kuwa vyama lazima viendeshwe kwa misingi ya vikao, si kwa maamuzi ya mtu mmoja, na kuelekeza kila chama kuwa na mpango kazi wa mwaka, mpango mkakati wa muda mrefu kama wa miaka mitano, pamoja na taarifa za mapato na matumizi.
“Utawala bora unaleta uwazi kwa wanachama na huongeza imani yao kwa uongozi. Hii huongeza ufanisi na kuleta tija katika maeneo ya kazi,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi mabaya ya fedha na migogoro ya kiuongozi huathiri moja kwa moja maslahi ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na mishahara, mafao, na mazingira bora ya kazi.
Katika maelezo yake, Wambali ametoa rai kwa vyama vya wafanyakazi kuachana na uanaharakati wa zamani na kuingia katika majadiliano ya wazi na waajiri kuhusu maslahi ya wafanyakazi.
“Vyama vitambue kuwa kazi yao kubwa ni kulinda maslahi ya wafanyakazi, si ya viongozi,” amesema.
Amesisitiza pia umuhimu wa utatu baina ya serikali, waajiri, na vyama vya wafanyakazi katika kujenga uchumi imara na jamii yenye ustawi.
Amesema vyama vya wafanyakazi vina mchango mkubwa si tu katika kukuza uchumi, bali pia katika kuweka mazingira bora ya kazi, mshikamano, na maisha bora kwa wafanyakazi.
“Tusijenge vyama kwa ajili ya viongozi. Tuyajenge kwa ajili ya wafanyakazi na maendeleo ya taifa,” amesisitiza Wambali.