Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAKULIMA wa zabibu katika Kata ya Mpunguzi, jijini Dodoma wamekiri kuwa, upatikanaji wa soko la bidhaa zilizoongezwa thamani za zao hilo ni mkubwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Zabibu na Masoko Mpunguzi (UWAZAMAM) Moses Masasi amekiri hilo kwenye mafunzo kwa Wakulima wa Zabibu yanayotolewa kwa siku mbili na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo cha Makutupora.
Mafunzo hayo yana lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.

Amesema kuongezeka kwa uhakika wa soko kunatokana pia na uongezaji thamani wa zao hilo katika upande wa usindikaji wa mvinyo.
Pia amesema, kabla hawajapata mafunzo kutoka TARI walikuwa wakizalisha wastani wa tani Moja na nusu kwa ekari lakni baada ya kupata mafunzo kutoka kwa Watafiti wanazalisha wastani wa tani nne hadi sita kwa ekari.

Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi kutoka kituo cha TARI Makutupora, Dainess Sanga amesema lengo la mafunzo hayo ni kufundisha kanuni bora za Kilimo cha zao hilo ili kuongeza tija zaidi kwa wakulima katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Sanga amesema pia kuongeza thamani katika zao hilo ili kuongeza tija kwa wadau wa kilimo badala ya kutegemea kuuza Zabibu ghafi pekee.
