Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: WAKULIMA wa mahindi Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro wameiomba Serikali kupitia watafiti wake kutafuta suluhisho la kudumu la namna ya kuwakabili viwavi jeshi vamizi wanaoharibu zao la mahindi, huku familia zikikabiliwa na njaa pamoja na umaskini.
Wakizungumza na watafiti wa Mradi wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima Katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo (AGRISPARK) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wilayani humo wamesema kila mwaka hali inakuwa mbaya kwa kushindwa kuwadhibiti wadudu hao hatari,
Ambao sasa wanashambulia na mazao mengine ya kijani pale mahindi yanapokauka shambani.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine, Mkulima wa mahindi kutoka Kata ya Wami Dakawa wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Salehe Mwendi amesema kwa sasa kilimo kimekuwa kigumu, changamoto za wadudu na ukame vinawaacha masikini wakulima wengi kwenye maeneo mengi.
“Jamani tunaiomba serikali kupitia watafiti wake na mamlaka zingine zenye uwezo wa kusaidia kupata ufumbuzi wa wadudu hawa, miaka ya nyuma tulizoea ukilima mahindi unasubiria kuvuna lakini kwa sasa hali imekuwa mbaya sana bila kupuliza dawa hupati chochote shambani,
“Tunatumia nguvu kubwa kulima lakini wadudu wanatunyima mazao yetu hasa kwa sisi ambao hatuna uwezo wa kununua dawa,” amesema.
Amesema, “Kwa sasa tunalima shamba tunapanda na kuhudumia kwa kupalilia kisha tunaacha wadudu wale na kile watakachobakisha shambani ndicho na sisi mwisho tunaenda kuokoteza na kurudisha nyumbani kula na familia yetu,
“Maana tulikimbilia kwenye zao la mpunga ambalo nalo haliathiriwi na wadudu hawa lakini sasa kwa miaka mitatu mfululizo ndege wanakuja makundi kama mchanga wakishuka shambani siku moja wanamaliza hata ekari 12, yani tunateseka sana,”.
Naye mkulima mwingine Mzee Mohamed Kigonile ameomba watafiti wa Mradi wa AGRISPARK – SUA waandike vitabu na juu ya elimu sahihi ya kukabiliana na wadudu hao,vinavyoweza kutoa maelekezo sahihi ya namna ya kufanya ili kuokoa mazao yao.
“Tunajua ninyi watafiti kutoka kwenye Chuo chetu kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) mnafanya kazi nzuri na tafiti nzuri kutusaidia wakulima tuzalishe kwa tija,
“Sasa tusaidieni kama kuna tafiti mlizofanya kuhusu wadudu hawa mtuletee tujifunze ili zitusaidie kuwatokomeza maana kwa uwezo wetu sisi tumefika mwisho tunahitaji msaada wenu na serikali. Mtuokoe njaa itatumaliza,” amesema.
Akizungumzia tatizo hilo Mtafiti Mkuu Mwenza wa Mradi wa AGRISPARK kutoka SUA Dkt. Nicholaus Mwalukasa amewaambia amepokea maombi yao, wanakwenda kutafuta machapisho ya kisayansi mbalimbali ambayo yamefanyika kuhusu namna ya kupambana na wadudu hao,
Wakiyapata wataandika vitabu vidogo ambayo vitaelezea na kufundisha namna ya kuwadhibiti wadudu hao.
“Tulipokuwa kwenye Kata ya Nyandira pia wakulima wametoa kilio hicho kwa wadudu hao katika zao la mahindi hivyo sisi kama watafiti tunalichukua na kwenda kulifanyia kazi maana tunamini zitakuwepo tafiti ambazo zimefanyika na kuchapishwa kwenye majarida ya kisayansi ya kimataifa ambayo sio rahisi nyinyi kuyafikia,
“Lakini sisi tutafanya hivyo kwa niaba yenu na kuwaletea kwa lugha rahisi ili muweze kuelewa,” amesema.
Watafiti hao wa mradi wa AGRISPARK kutoka SUA wametembelea wakulima kwenye wilaya ya Mvomero, Morogoro Manispaa na Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini na kukutana na wakulima na kuungumza nao kuhusu mahitaji yao ya elimu kwenye shughuli za kilimo.
Pia changamoto zinazowakabili ili waweze kuwatafutia ufumbuzi wa changamoto zao kwa kuandaa vitabu vidogo vya kuwaelimisha kuhusu mahitaji yao.
Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na serikali kupitia SUA ikiwa ni maono mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwa ajili ya kuwawezesha watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.