Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Masoud Muruke ametoa wito kwa Wajumbe wa tume hiyo kutembelea ofisi za ngazi ya Wilaya zilizopo karibu na maeneo yao kwa lengo la kupata maoni na kufahamu changamoto zinazowakabili watumishi.
Muruke ametoa kauli hiyo wakati akiendesha Mkutano wa TSC unaofanyika mjini Morogoro.
Amesema kuwa Wajumbe wa Tume wana wajibu wa kusimamia na kuhakikisha Ofisi zote za TSC zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutoa huduma kwa walimu.
“Mimi mwenyewe jana niliona ni vema kutembelea Ofisi za Tume Wilaya ya Morogoro kwa kuwa nipo hapa Morogoro.
“Tukitembelea ofisi zetu hizi tunapata fursa ya kufahamu mazingira ya kazi ambayo wenzetu wanafanyia kazi. Pia, inasaidia kupata maoni yao na kufahamu changamoto zinazoweza kukwamisha utoaji wa huduma bora kwa walimu,” amesema.
Amesema katika kutembelea ofisi hizo, itssaidia kuwa katika mazingira mazuri ya kufanya uamuzi sahihi kwa maslahi ya maendeleo ya walimu.