Na Danson Kaijage
DODOMA: WAHITIMU wa Kidato cha Nne mwaka 2024 wamepata fursa ya kubadilisha machaguo ya tahasusi za Kidato cha Tano, Vyuo vya Kati na Elimu ya Ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano na vyuo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, ameeleza hayo
alipozungumza na Vyombo vya Habari jijini Dodoma.

Amesema hatua hiyo ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha tano na Vyuo vya Serikali Mwaka, 2025.
“Itakumbukwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi na kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi.
“Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA),” amesema.

Mchengerwa amesema, serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imekamilisha kazi ya awali ya kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye fomu za uchaguzi za wanafunzi kama walivyozijaza wakiwa shuleni.
Amesema kukamilika kwa kazi hiyo kunatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo, tahasusi ama kozi kwa njia ya mtandao.
“Baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye.
“Zoezi hili litatoa fursa zaidi ya wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya Tahasusi na Kozi.
“Napenda kuwasihi wazazi, walezi kushiriki katika jambo hili kwa kushauriana na watoto wao katika kufanya machaguo sahihi kulingana na ufaulu wao,” amesema.
Amesema wahitimu wote wanahimizwa kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.
Amesema kazi hiyo ya kubadilisha
tahasusi na vyuo litaanza rasmi Machi 31 Machi, 2025 hadi Aprili 30 2025.