Na Lucy Ngowi
DODOMA:SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema uzinduzi wa miongozo na mifumo ya kielektroniki ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, inaweka historia mpya kwa wafanyakazi nchini.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), Rashid Mtima aliyemwakilisha Katibu Mkuu TUCTA, Very Mkunda amesema hayo wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma.

Mtima amesema uzinduzi huo unaweka historia kwa sababu mifumo hiyo inaleta uwazi na uwajibikaji zaidi katika utendaji wa wizara hiyo muhimu.
“Wafanyakazi wa Tanzania wanajivunia hatua hii muhimu. Miongozo na mifumo hii ya kielektroniki si tu kwamba inarahisisha kazi, bali pia inaleta utaratibu na uwazi unaotegemewa katika usimamizi wa kazi na ajira nchini,” amesena.
Ameongeza kuwa miongozo hiyo ni sehemu ya kutekeleza mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), na hivyo Tanzania inaendelea kuonesha mfano mzuri wa utekelezaji wa haki na usawa mahali pa kazi kimataifa.
Mtima amesisitiza kuwa mifumo hiyo itawezesha majadiliano ya wazi kati ya serikali, waajiri na wafanyakazi, jambo ambalo halikuwepo kwa uwazi wa kiwango hicho hapo awali.
“Tumeweka historia kwa kuweka mifumo rasmi ya majadiliano, jambo ambalo halikuwahi kutekelezwa kwa uwazi huu. Sasa wafanyakazi wanapata mwongozo wa wazi kuhusu haki zao na wajibu wao, na hii ni hatua kubwa sana,” amesema.
Wafanyakazi nchini pia wamepongeza juhudi za serikali kurahisisha namna ambavyo wadau mbalimbali wanashirikiana, hasa katika kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha mazingira bora ya kazi.
Katika hatua nyingine, Mtima amewaasa wafanyakazi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha maslahi ya wafanyakazi, akitolea mfano ongezeko la asilimia 35 la mishahara ambalo limekuwa ni la kihistoria.
“Hatujawahi kuona ongezeko la asilimia 35 kwa mara moja, na hii inaonesha dhamira ya kweli ya serikali katika kuimarisha maisha ya wafanyakazi. Tunatambua na kuthamini sana hatua hiyo,” amesema.