Na Lucy Ngowi
DODOMA: VIFAA 3,050 vya kupima ulevi kwa madereva vimetolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa Jeshi la Polisi nchini kwa ajili ya kusaidia kudhibiti ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva walevi na wazembe, pale wanapoendesha pasipo kuzingatia sheria.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura akipokea vifaa hiyo amesema, jeshi hilo limeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ajali za barabarani ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyokuwa akiyatoa mara kwa mara ya kuhakikisha ajali za barabarani zinadhibitiwa ipasavyo.
Wambura amesema kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani watakuwa wakali kwa madereva wazembe ambao wamekuwa wakisababisha ajali za barabarani ikiwa ni Pamoja na kutoa elimu hiyo kwa jamii ili kuhakikisha watanzania wanakuwa salama.
“Tumeweza kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali na sasa nguvu pia tunazielekeza kwenye usalama barabarani kwa kuwa takwimu za ajali bado zipo juu hivyo ni lazima tuwe wakali sana ili kuona sheria za usalama barabarani zinafuatwa ili kuokoa maisha ya Watanzania,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo amesema utendaji kazi wa mamlaka hiyo unahitaji ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kusimamia Sheria za Usalama barabarani.
Amesema vipima ulevi hivyo vitasaidia kikosi hicho kudhibiti ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva walevi na wazembe pindi wanapokuwa barabarani na kuendesha pasipo kuzingatia sheria.
Suluo amesema uwepo wa vifaa hivyo utasaidia kupima madereva mara kwa mara wawapo barabarani jambo ambalo litasaidia kufanya barabara kuwa salama.
Pia amesema mamlaka hiyo itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutumia mifumo katika kufanya ukaguzi wa magari ambapo kwa sasa wanaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali.