Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji Serikalini kuhakikisha vipaumbele vilivyoanishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026 vinatafsiriwa vema kwenye mipango ya taasisi zao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Novemba nane, 2024 wakati akiahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma, ambapo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026.
Amesema mpango huo umejikita katika kuendeleza na kukamilisha utekelezaji wa afua zinazotoa matokeo ya maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

“Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi itaweka mkazo katika maeneo ya miradi ya kielelezo yenye manufaa na matokeo makubwa na kujielekeza katika vipaumbele vya mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026.” amesema
Amesema vipaumbele hivyo ni: kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimaliwatu.