Na Lucy Lyatuu
CHAMA Cha Sauti Ya Umma (SAU) kimeshauri kuwepo kwa jukwaa litakaloshirikisha viongozi wa din izote nchini wakijifungia ndani na kufanya maombi kisha kujadili kwa haraka kuhusu hali iliyopo na kutoa mapendekezo yao kwa wananchi.
Katibu Mkuu wa SAU, Majalio Kyara ambaye alikuwa mgombea Urais kupitia chama hicho, amesema hayo Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 pamoja na vurugu zilizotokea.
Amesema hiki kipindi sio cha kuongea sana bali ni wakati wa kujifungia kutafakari, na ili kujua kipi kifanyike na kwa nini Taifa limefika lilipo lengo likiwa ni kutatua changamoto.
“Wote tunawakubali viongozi wa dini ni rahisi wao wakieleza jambo kueleweka, hivyo wakikaa wakijadili na kujua wapi kuna makosa itasaidia waliokosa kuomba radhi na kusamehewa,” amesema na kuongeza kuwa na hata vitabu vya dini vinaeleza ubaya usilipwe kwa ubaya bali wakiomba radhi wasamehewe.
Amesema ni vyema viongozi hao wakijadiliana kwa haraka sana kabla ya Novemba 25, 2025 ili isifikie huko wanakoeleza 9 Desemba.
“Na hii ningependa tuwatumie zaidi viongozi wa dini, tunaamini hivyo kila mtanzania asilimia 99 ni muislamu au mkristo ambapo viongozi hao wametubeba sisi kwa asilimia kubwa, tukitumia vyama kuna wengine hawana vyama hivyo, tutafute jukwaa la viongozi wetu wa dini zote wote wajifungie ndani, waelezwe na wananchi ambao nao wameshakutana nao wakijua nini kilichotokea na vyombo vya ulinzi vinaweza kuwaeleza yaliyotokea,” amesema.
Amesema hekima na busara za viongozi hao kwa kuwa watakuwa ndani wanaelezwa watapata picha kama kuna watanzania walitaka kuwa wasaliti wataelezwa na kwa pamoja wote watatoka kwa wananchi kwa msimamo mmoja.
Kyara amesema ni lazima kumtanguliza Mungu mbele akionesha njia, ya namna ya kutoka mahali Taifa lilikofikia kwa maana hata Rais Samia Suluhu Hassan alisema fujo zilizotokea zimetia doa.

