Na Mwandishi Wetu,
KILIMANJARO: VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga wameibua hoja saba za msingi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu 2025 wakisisitiza amani, haki na busara kwa vyombo vya dola.

Wakizungumza katika Kongamano la Amani lililofanyika katika ukumbi wa Uhuru Hostel, Moshi, viongozi hao wakiwemo Masheikh, Maaskofu, Mapadri na Wachungaji wametoa wito kwa Watanzania kuendeleza umoja na kuwapuuza wanaohamasisha vurugu.
Katibu wa BAKWATA mkoa wa Kilimanjaro, Alhaji Awadhi Lema, akisoma maazimio ya kongamano hilo, amesema viongozi wa dini wamekubaliana kuhimiza wananchi kuhakiki majina yao na kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani.
Amesema pia wameazimia kuendelea na makongamano ya amani, kuelimisha waumini kuhusu haki na wajibu wao, na kuonya dhidi ya uchochezi mitandaoni.
“Vyombo vya dola vinapaswa kutumia busara na hekima kulinda amani, hasa siku ya uchaguzi,” amesema Lema.
Aidha, viongozi hao walipendekeza viongozi wa dini washirikishwe zaidi katika vyombo vya maamuzi na kutunga sheria, huku wakisisitiza kila raia ana wajibu wa kulinda amani wakati wa kudai haki.
Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Shaban Mlewa, amesema Watanzania wanapaswa kujifunza kutoka kwa mataifa yaliyopoteza amani, akisisitiza umuhimu wa uzalendo, upendo na uadilifu.
“Amani ni urithi muhimu, tusiiache ipotee mikononi mwetu,” amesema.
Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaban Juma, ameongeza kuwa haki haiwezi kupatikana bila amani.
“Amani inajengwa kwa kumcha Mungu, kujitambua na kulinda uhai wa wengine,” amesema.
Kwa upande wake, Wakili Mchungaji Daniel Swai wa KKKT Kaskazini amesema ni kosa mtu kuhamasisha wengine kutopiga kura, akisisitiza haki na amani haviwezi kutenganishwa.
Padri Deogratias Matiika wa Jimbo Katoliki la Moshi amewataka wananchi na viongozi kuheshimiana na kuepuka matusi mitandaoni.
“Kuheshimu haki ni msingi wa utulivu wa taifa,” amesema.
Padri Francis Mahimbo wa Kanisa la Anglikana Tanga amewataka Watanzania kuendeleza uvumilivu na kuheshimu haki za binadamu ili taifa liendelee kuwa na amani.
Kongamano hilo pia liliwahusisha kamati za dini za wanawake na vijana, ambazo ziliwataka Watanzania kushiriki uchaguzi kwa amani na kuwakataa wanaotaka kuchochea vurugu au uvunjifu wa sheria.

