Na Lucy Ngowi
DODOMA: UZIDISHAJI wa uchanganyaji wa chakula cha mifugo ni changamoto inayowakabili wafugaji wengi nchini.
Mwalimu wa Fani ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji kutoka Chuo cha Ufundi Stadi ( VETA) mkoani Singida., Ladslous Chemele amesema hayo katika maonesho ya Nanenane ya Kitaifa na Kimataifa yanayoendelea mkoani Dodoma.

Amesema malighafi zinazotumika kutengeneza chakula cha mifugo zimegawanyika katika makundi matatu, na kila kundi lina kiasi maalum kinachotakiwa kuzingatiwa kulingana na aina ya mnyama na hatua ya ukuaji aliyonayo.
“Ukizidisha kwa vifaranga, protini inazidi kiwango kinachotakiwa, na hilo huleta madhara kiafya. Kwa kuku wanaotaga, wakinenepa kupita kiasi ovari hujaa mafuta na hushindwa kutaga vizuri. Vilevile, chakula kikipungua virutubisho, huweza kukosa madini au kutaga yai na kulila,” amesema.
Kwa upande wa ng’ombe wa maziwa, Chemele amesema kuwa iwapo hawatapata chakula bora chenye virutubisho vya kutosha, miili yao hupungua uzito na uzalishaji wa maziwa hushuka.
Pia amesema chuo hicho hutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa Watanzania wanaopenda kujifunza masuala ya afya ya mifugo na uzalishaji.
Chemele ameeleza kuwa mafunzo ya muda mrefu huchukua miaka miwili hadi mitatu, na ya muda mfupi huanzia miezi miwili na kuendelea. Mafunzo hayo yanatolewa kwa kila Mtanzania mwenye nia ya kujifunza.
Amesema wanafundisha utengenezaji wa chakula cha kuku wa mayai, wa nyama, chotara na wa kienyeji
Vile vile chakula cha ng’ombe wa maziwa na wa nyama kama chakula cha ziada, Utengenezaji wa chakula cha nguruwe, bata maji na njiwa.
Chemele amesema mtu yeyote anayefika chuoni hapo hufundishwa kwa kuzingatia miongozo sahihi ya kutengeneza chakula chenye ubora kwa mifugo, kwa kutumia viwango vinavyokubalika kitaalamu.