Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeanzisha kozi mpya ya Teknolojia ya Mifumo ya Viwandani ‘Mechatronics’ katika baadhi ya vyuo vyake, ikiwemo Chuo cha VETA Kipawa kilichopo Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu kozi hiyo, katika kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), mtaalamu wa fani hiyo, Joshua Kingu kutoka VETA Kipawa MKoani Dar es Saalam amesema,

Kozi hiyo ni ya kisasa na inalenga kutoa ujuzi wa kiteknolojia unaoendana na mahitaji ya sasa ya viwanda.
Amesema zamani mitambo mingi ya viwandani ilikuwa inaendeshwa na binadamu, lakini sasa imebadilika na kuendeshwa na mifumo ya kielektroniki na kompyuta.
Amesema mabadiliko haya yamezua hitaji kubwa la wataalamu waliobobea katika teknolojia ya mechatronics.
Ameeleza kuwa kozi hiyo inalenga kuwapa wanafunzi wa VETA na watu wazima ujuzi wa kisasa, ili wanapopata ajira viwandani wawe tayari kufanya kazi kwa vitendo na kuendana na teknolojia mpya.
“Mitambo ya kisasa, kama ile inayotumika kwenye viwanda vya maji na saruji, imekuwa ya kielektroniki zaidi.
Wafanyakazi wanapaswa kuwa na uwezo wa kufunga, kutengeneza, na kutatua matatizo ya mitambo hiyo,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Habari na Uhusiano wa VETA, David Mpondyo, amesema lengo la mamlaka hiyo ni kuwafikia Watanzania wote wanaotaka kupata mafunzo ya ufundi, bila kujali kiwango chao cha elimu au ujuzi wa awali.
“Tunataka kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, hasa katika kipindi hiki cha ukuaji wa viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa,” amesema Mpondyo.
Amesisitiza kuwa zamani baadhi ya viwanda vililazimika kuagiza wataalamu kutoka nje kufundisha wafanyakazi wao, lakini sasa VETA inatoa mafunzo hayo nchini, jambo linalosaidia kupunguza gharama.
Mpaka sasa, VETA ina jumla ya vyuo 80 vya ufundi vilivyopo kwenye kila mkoa nchini, na vingine 65 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
“Kozi hii mpya haijamlenga kijana mwenye ujuzi tu, bali pia wale ambao hawajawahi kupata nafasi ya kujifunza. Lengo ni kuwaandaa vijana kujiajiri, kuajiriwa, au hata kuwaajiri wengine,” amesema Mpondyo, na kuongeza kuwa VETA itaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia bunifu ili kuchochea maendeleo ya viwanda hapa nchini.