Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAJASIRIAMALI wanaofanya kazi katika saluni za kike na kiume, wameshauriwa kusoma Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ili kuongeza ujuzi na maarifa katika kazi yao hiyo.
Ushauri huo umetolewa na Mwalimu wa Saluni, Mapambo na Urembo kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, Juddy Mwita alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania katika Maonyesho ya Sabasaba ya mwaka huu 2025, yanayoendelea Mkoani Dar es Salaam.
Amesema, ” Nipo hapa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa umma pia kuwaeleza umuhimu wa kutumia vitu vya asili kama mafuta ya kujaza nywele, sabuni za mchele,mwarobaini na mwani,”.
Amesema wale ambao hawajasoma VETA wamekuwa wakitumia bidhaa kinyume na inavyotakuwa.
“Mfano vifaa kama drier na mashine nyingine hutumika vibaya kwenye saluni kwani kuna watu ambao hawatakiwi kukaa kwenye mashine lakini wanawekwa.
” Kupaka zile dawa kuna kanuni zake. Kuna mtu anapakwa dawa inatakiwa aoshwe na maji ya uvuguvugu lakini anaoshwa na ya baridi,” amesema.
Amesema matumizi mabaya ya bidhaa yanaathiri binadamu, kwani kuna watu wanatumia mafuta na kwa kuwa hawajui matumizi yake kwa usahihi yanawaathiri.
Amesema watu hao wakipata mafunzo watayatumia vizuri katika kazi zao.
Amesema pia wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi wao ujasiriamali kwa kuwaonyesha jinsi ya kutengeneza bidhaa za asili ikiwa ni pamoja na namna ya kuwakaribisha wateja.
“Nawakaribisha watu wa saluni waje wapate elimu ili waendeshe saluni zao vizuri. Mtu asifungue saluni bila kupata mafunzo,’ amesema.