DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imepewa maelekezo mahsusi ya kujenga mahusiano na wenye viwanda na wazalishaji wa bidhaa ambazo zinahitaji ufundi au ufundi stadi.
Profesa Mkenda amesema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya miaka 30 ya VETA pamoja na miaka 50 ya utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia taasisi mbalimbali za serikali nchini
Amesema, “Maadhimisho hayo yamekuja wakati mamlaka hiyo ina maelekezo mahsusi ya kujenga mahusiano na wale wenye viwanda na wazalishaji wa bidhaa ambazo zinahitaji ufundi au ufundi stadi ambao unatolewa VETA,”.
Amesema wamekubaliana na mamlaka hiyo kwamba ndani ya miezi mitatu itakuwa na ‘frame work’ ya mahusiano kati ya vyuo vya VETA na viwanda au wazalishaji wa bidhaa zinazohitajika nchini ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa mamlaka hiyo kujifunza kwa vitendo,
Kwa wazalishaji au wenye viwanda kusaidia kutoa mafunzo kwa vijana na vile vile kunufaika na uwepo wa nguvu kazi hiyo katika vyuo.
“Utaratibu huu utahusisha na urasimishaji wa utaalam uliopo katika maeneo mbalimbali ya viwanda au uzalishaji,
“Kwa mfano wako watanzania sasa hivi wanatengeneza suti nzuri kwa muda mfupi ambazo zina hadhi ya kimataifa ni wajuzi ni wabunifu inawezekana hawajasomea mahali popote ubunifu wakati mwingine ni utundu wa mtu tunawahitaji hawa waweze kutusaidia katika vyuo vyetu vya VETA,
“Kwa kuwachukua vijana wanaosoma katika vyuo vyetu kufanya nao kazi wajifunze kutoka kwa hawa watu mahiri wachukue utaalam wao kwa vitendo na wakati huo huo watoe nguvu kazi kwa wazalishaji ili waweze kuzalisha kwa wingi zaidi kuhakikisha tunakidhi soko la ndani hata kwenda kuuza nje ya nchi,” amesema.
Waziri Mkenda amesema ili kufikia huko lazima kuwe na makubaliano maalum na utaratibu wa wazi ambao unaruhusu yeyote mzalishaji au mwenye kiwanda anaweza akaingia katika utaratibu huu kwa ushindani unaokubalika.