Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: UZINDUZI wa ushirikiano wa wabia katika Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025, Umefanyika leo mkoani Dar es Salaam.
Wabia hao ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) Tanzania, Vodacom Tanzania na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH).
Mkuu wa Uhusiano na Vyombo vya Habari Vodacom Tanzania, Annette Kanora amesema uzinduzi huo umefanywa na wabia muhimu katika eneo la teknolojia.

Amesema UNDP kupitia Program ya Ufunguo Innovation, COSTECH na wao Vodacom Tanzania wamezindua ubia huo kwa ajili ya wiki hiyo ya ubunifu itakayofanyika Mei 12 mpaka 16, Dar es Salaam.
“Wiki ya ubunifu ni jukwaa linaloleta pamoja taasisi mbalimbali, wabunifu mbalimbali katika kupeleka tasnia nzima ya ubunifu na teknolojia hapa Tanzania.
“Kupitia ubia wao kama Voda tunaongeza nguvu, tunapata wazungumzaji mbalimbali toka ndani na nje ya nchi ili tuweze kubadilishana uzoefu wengine wanafanya nini.
“Tunaenda kujenga taifa ambalo ni endelevu, na linakuwa ni la kibunifu,” amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya Funguo Innovation ambayo ipo chini ya UNDP inayoshirikiana na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Uingereza, Joseph Evarest amesema ubia uliozinduliwa utakuwa ni jukwaa la kuonyesha nini kinafanyika katika eneo la ubunifu na teknolojia.

“Tunaamini kupitia ubunifu kuna biashara nyingi zinachipuka, kuna biashara mpya, kuna teknolojia nyingi zinakuja kwa hiyo ni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali ambao wako katika nafasi hiyo kuonyesha wanafanya nini.
“Lakini vile vile kusikiliza kuna mahitaji gani ya kiubunifu na kiteknolojia katika nafasi ya Tanzania.
“Tunajua Tanzania inakuwa kwa kasi sana na uchumi unabadilika. Shabaha ya Funguo ni kusaidia vijana wanaibua biashara bunifu katika mitaji, msaada wa kiufundi pia masuala ya kusera yaliyopo ambayo yanakwamisha,” amesema.

Naye Kiongozi katika Mashirikiano, Promise Mwakale kutoka COSTECH amesema ubia walioingia utanufaisha vijana kwa kuwa Wiki hiyo ya ubunifu itakuwa na majadiliano kwa ajili yavwanafunzi, pia itawawezesha kupata nafasi mbalimbali.
“Huu ni muda wa kukutana na wabunifu. Kama COSTECH tuna furaha kuwa sehemu ya huu ushirikiano kwa kuifanya Wiki ya Ubunifu kuwa Kubwa zaidi,” amesema.
