Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MHADHIRI Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOM), Dkt. Benatus Mvile amesema roketi wanayoifanyia utafiti chuoni hapo sasa imekuwa na uwezo wa kuruka kwenda kwenye njia wanayoitarajia.
Dkt. Mvile amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania kuhusu hatua iliyofikia roketi hiyo ambayo chuo cha UDOM kimeifanyia utafiti kwa lengo la kutoa majibu chanya kwa jamii inayoizunguka.
Amesema, ” Roketi ya mwaka jana tuliyokuja nayo kwenye maonesho ya sabasaba ilikosa uhimilivu, ilikuwa haina uwezo wa kuruka kwenda kwenye njia tunayoitarajia, lakini sasa imekuwa himilivu,”.
Amesema chuo hicho kimekusudia kufanya mwendelezo wa mradi huo kufikia hatma yake na kuweza kuirusha.
“Moja ya changamoto ambayo tulipata mwaka jana ni kuiwezesha roketi hii kuwa himilivu,” amesema.
Amesema kwa mwaka huu, wameweza kuifanyia roketi hiyo maboresho ya mabawa ya nyuma na muonekano wake wa mbele.
Akielezea umuhimu wa roketi kwa jamii, amesema katika kipindi hiki kumekuwa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, na kusababisha uzalishaji wa chakula kupungua kwa kiasi kikubwa huku idadi ya watu ikiongezeka.
“Sasa mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanasababisha mvua isinyeshe kwa wakati, au kwa kiwango kinachostahili ni lazima tutafute njia mbadala ya kuwezesha mvua kunyesha kwa kiwango kinachotakiwa.
“Moja ya teknolojia inayotumika ni roketi ambazo zinasaidia kwenye masuala urekeboshaji wa hali ya hewa ili kuwezesha mvua ziweze kunyesha kwa kiwango kinachostahili,” amesema.
Amesema kwa namna hiyo kama chuo wanaenda kuigusa jamii kubwa na ya kawaida, kwa sababu wazalishaji wakubwa ni wakulima wa kawaida ambao hawana uwezo wa teknolojia za kisasa kama za umwagiliaji na kuchimba visima.