Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: OFISI ya Taifa ya Takwimu ( NBS), inafanya utafiti nchi nzima katika maeneo ya ajira, mapato ya kaya, huduma za kijamii, na matumizi ya nishati safi.
Aidha utafiti wa kitaifa wa nguvu kazi unaendelea, ukikusudia kutoa takwimu sahihi kuhusu watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini kujua umri wao, jinsi na maeneo wanakoishi.
Ofisa Masoko Mwandamizi wa Takwimu wa NBS, Andrew Punjila amesema hayo katika Maonesho ya 49 ya Kitaifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yaliyomalizika jana Julai 13, 2025 mkoani Dar es Salaam.
Amesema utafiti huo ni nyenzo muhimu kwa Serikali katika kupanga na kuboresha mikakati ya ajira, ikiwa ni pamoja na programu za kukuza ajira katika sekta mbalimbali.
Amesema NBS imeendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu rasmi kupitia maonyesho mbalimbali.
Pia amesema taarifa kutoka kwenye sensa na tafiti zingine zinaonyesha hali ya kijamii katika jami ikiwa ni pamoja na hali ya elimu, huduma za afya, nishati safi, na changamoto kama ukataji miti unaochangia uharibifu wa mazingira.
“Tunazo takwimu za hali ya uoto wa asili kuanzia mwaka 2002 hadi 2022, ambazo zinaonyesha kupungua kwa misitu na uoto wa asili kutokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
“Serikali kwa sasa inahamasisha matumizi ya nishati safi, na takwimu hizi zina msaada mkubwa katika kubaini maeneo yenye changamoto zaidi na kuweka mikakati ya kuboresha hali hiyo,” amesema Punjila.
Amesena NBS inatekeleza utafiti wa mapato na matumizi ya kaya ambao unapita kaya kwa kaya katika maeneo yote ya nchi, hadi kwenye ngazi ya maeneo ya kuhesabia.
Utafiti huo unalenga kutoa picha ya ustawi wa jamii, upatikanaji wa huduma za kijamii, na hali ya kiuchumi ya Watanzania.
Amesema takwimu hizo pia hutumika katika kukokotoa mfumuko wa bei, hali ya umasikini, na viashiria vingine vya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuvitumia vyanzo hivyo vya taarifa kwa ajili ya maendeleo binafsi na ya kitaifa.
Amevitaka vyombo vya habari kushirikiana na NBS katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa takwimu rasmi, kwa kuwa ni msingi imara wa mipango yenye tija.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Mfumo wa Taifa wa Kijiografia NBS, Andrew Gondwe amesema ofisi hiyo huzalisha takwimu muhimu za kijiografia ambazo huchambua hali ya upatikanaji wa huduma mbalimbali kama vile elimu, afya, maji, na hata huduma za kifedha katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesisitiza umuhimu wa wadau, wakiwemo wawekezaji na watunga sera, kutumia takwimu hizo katika kupanga maendeleo.
“Takwimu hizi si tu kwa ajili ya Serikali. Zinawafaa pia wajasiriamali na wawekezaji. Kwa mfano, mfanyabiashara anaweza kutumia takwimu hizi kupanga mahali pa kufungua huduma fulani kulingana na upatikanaji au ukosefu wa huduma hiyo katika eneo husika,” amesema Gondwe.