Na Mwandishi Wetu
DODOMA: TAKWIMU za elimu na ajira duniani zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake na wasichana katika elimu na ajira katika fani za sayansi ni mdogo ikilinganishwa na ushiriki wa wanaume.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga amesema
hayo leo Februari saba, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya maadhimisho ya Kitaifa ya wanawake na wasichana katika Sayansi ambayo huadhimishwa kila ifikapo Februari 11.
Kipanga amesema kwa takwimu za Tanzania ushiriki wa wanawake ni asilimia 36 na wanaume ni asilimia 64, hali inayopunguza juhudi za kufikia usawa.
Amesema mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknologia Profesa.Adolf Mkenda,
Amesema lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake na wasichana katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).
Pia amesema maadhimisho haya ni fursa ya kuhamasisha wanawake na wasichana zaidi kujiunga katika nyanja hizi ili kubadili mustakabali wao na jamii zetu kwa ujumla.
“Baraza Kuu la Umoja wa MATAIFA mwaka 2015, lilipitisha programu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kwa kutangaza tarehe 11 Februari kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika sayansi.,”ameeleza.
Amesema Tanzania inatambua kuwa usawa wa kijinsia ni muhimu sana kwa kufikia malengo ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Kipanga amesema kutokana na maazimio hayo ya Umoja wa mataifa, Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kuanzia mwaka 2021.
“Masuala ya wanawake na wasichana ni mtambuka, hivyo yanahitaji ushiriki na mchango wa wadau wote bila kujali wako katika sekta ya umma au binafsi,
“Tnahitaji kuhamasisha kizazi kilichopo na kijacho cha wasichana kupenda na kujiunga na masomo ya sayansi kwa kuondoa dhana potofu na kutoa fursa sawa katika elimu na maendeleo ya kitaaluma”amesema.