Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Afya ya Mmea na Viuatilifu (TPHPA), imewezesha usafirishaji wa shehena za mazao mbalimbali tani milioni 3.5 kwenda nje ya nchi, kupitia ukaguzi wa mipaka.
Aidha usafirishaji wa shehena hizo umeingizia Tanzania Dola Bilioni 3.54 kwa mwaka kupitia ukaguzi unaofanywa mipakani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mmea na Viuatilifu (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi Tanzania.
Profesa Ndunguru amesema pia mamlaka hiyo imekamilisha nyaraka za kufungua masoko kwa mazao tisa katika nchi 14 ambazo tayari nyaraka hizo zimekabidhiwa balozi za nchi husika.
“Ufunguaji wa masoko hayo utaingizia Tanzania kiasi cha Dola Bilioni 3.5 kwa mwaka.
“Uwezeshaji wa masoko tayari shehena ya kwanza ya parachichi imesafirishwa kwenda China,” amesema.
Kwa upande mwingine Profesa Ndunguru amesema, mamlaka hiyo imewezesha upatikanaji taarifa za kufungua masoko kwa mazao tisa katika nchi 14.
Ameyataja mazao hayo kuwa ni vanilla, soya, parachichi, mananasi, viazi mviringo na mengineyo.
Amesema taarifa hizo wameshapatiwa nchi husika na tayari taratibu za kuuza mazao kwenye nchi hizo zinaendelea.
“Kwa hiyo kwa sasa hivi mamlaka kwa kuwepo kwetu mipakani ofisi 36 hizo pamoja na mipaka ya nchi kavu na viwanja vya ndege sasa takwimu za mauzo ya mazao yanayoenda nje na kuingia ndani zinapatikana TPHPA.
“Sasa hivi unaweza kuitisha taarifa yoyote hata sasa hivi nikitaka kujua mpaka wa Tunduma mwezi huu wamepitisha mazao gani, wameingiza fedha kiasi gani unaipata kwenye kituo chetu cha Arusha.
“Kwa hiyo ukitaka kwa mwezi kwa mwaka utapata kila kitu, na kwa zao unapata data zake,” amesema.
Amesema data hizo zinatumiwa pia na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kupata majibu ya taarifa mbalimbali.