Na Danson Kaijage.
UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati umesema nafasi zilizoachwa na viongozi walioondoka, zitazibwa siku za karibuni.
Aidha uongozi huo umewatakia heri wanachama wote walioondoka katika chama hicho.
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa chama hicho Kanda ya Kati, Ashura Masoud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa kisiasa katika chama hicho.

Amesema suala la mwanachama kuhama chama na kujiunga na chama kingine ni jambo la kawaida na ni la kidemokrasia hivyo kila anayetaka kuondoka CHADEMA na kujiunga na chama kingine ruksa kwa kuwa chama hicho, siyo gereza la kuwafungia wanachama.
“CHADEMA ni taasisi na CHADEMA ni bora kuliko mwanachama hivyo kuna watu wameondoka ndani ya chama kwa kushindwa kufuata misingi ya chama chetu, CHADEMA inawatakia heri na wanatakiwa kujua kuwa CHADEMA ni imara sana.
“Tumeshuhudia uchaguzi wa 2019 wa Serikali za Mitaa ulivyokuwa wa ovyo,tumeshuhudia uchaguzi wa 2020 ulivyokuwa wa ovyo zaidi na sasa tunasema kama hakuna Tume Huru ya uchaguzi hakuna uchaguzi hatuwezi kuingia kwenye uchaguzi ili watu waumizwe kutokana na mifumo ya ovyo ya uchaguzi,” amesema.
Pia amesema chama hicho kimejaa hazina ya viongozi makini ambao wanaweza kuongoza tena kwa uhakika zaidi hivyo wale wanaoondoka kwa visingizio mbalimbali wanatakiwa kupuuzwa ili shughuli ya kimapambano iendelee.
Amesema inashangaza kusikia mwanachama aliyehama au anayehama akidai kuwa Chadema imepoteza misingi yake wakati kashindwa kusimamia misingi, hiyo inatokana na baadhi ya waliokuwa wanachama kutokuwa waumini wa chama bali ni waumini wa mtu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Dodoma Dkt. Stevine Karashani amesema inawezekanaje kiongozi ndani ya chama mwenye nafasi ya uongozi akadai kuwa chama hakina maono wakati yeye hupo ndani ya uongozi.
Amesema wapo waliokuwa wanachama ambao wamelelewa na chama hicho hadi kusafirishwa ughaibuni kwa ajili ya kupatiwa mafunzo lakini leo wanadai kuwa chama hakina maono hiyo ni aibu kwao kwani sasa wanatafuta kukubalika kwa nguvu.