Na Lucy Ngowi
GEITA: KATIBU Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohammed Gombati amesema unywaji wa maziwa safi na salama kwa wanafunzi wa shule ni hatua muhimu katika kuongeza ufaulu na kuboresha afya za watoto mkoani humo.
Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wadau wa Tasnia ya Maziwa, lililofanyika katika Ukumbi wa Nyerere, Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita, Gombati amesema maziwa ni chanzo bora cha lishe ambacho kitasaidia wanafunzi kuepuka udumavu wa mwili na akili.
“Walimu, wazazi na walezi wana jukumu kubwa kuhakikisha watoto wanapata maziwa shuleni. Zoezi hili lazima liwe endelevu ili kuleta matokeo chanya kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Gombati.
Kwa upande mwingine, Katibu Tawala huyo aliwataka maofisa lishe kuendelea kuelimisha jamii juu ya faida za lishe bora, hususan matumizi ya maziwa safi, huku akiagiza maofisa mifugo kuwahamasisha wafugaji kufuga kisasa ili kuhakikisha upatikanaji wa maziwa kwa mwaka mzima.
Katika kongamano hilo, Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Deorinidei Mng’ong’o, amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuandaa mpango maalum na endelevu wa kuhakikisha watoto shuleni wanapata maziwa kila siku ili kukuza ustawi wa afya zao na kuongeza uwezo wao wa kujifunza.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ilikuwa:
‘Kwa Matokeo Mazuri Shuleni na Afya Bora, Maziwa Ndiyo Mpango Mzima’.