Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAFUGAJI wameshauriwa kufuga sungura ili kupunguza gharama za kununua mbolea pamoja na dawa za kunyunyiza katika mazao kwa kuwa kinyesi na mkojo wake ni mbolea na dawa ya wadudu.
Mtaalam wa Maabara kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Julius Ngumba ameeleza hayo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea Jijini Dodoma.
Amesema, ” Sisi kama Chuo Kikuu tunaonyesha fursa kuwa ukifanya hivi utapata kitu fulani Ukifuga sungura sio kwa ajili ya nyama peke yake, bali nje ya nyama kinyesi ni mbolea na mkojo pia.
“Sungura anakojoa sana ukifuga sungura hutaingia gharama ya kununua dawa dukani bali ukitumia mkojo wake ni dawa ya wadudu,” amesema.
Amesema wadudu wakisikia harufu ya mkojo wa sungura hawawezi kukaa hukimbia, hivyo mkojo huo ukinyunyizwa utazuia wadudu wasitue kwenye mazao.
Anasema ili mkojo ufanye kazi ya kuzuia wadudu inashauriwa asilimia 75 kati ya 100 uwe mkojo na asilimia 25 iwe maji ndio uchanganwe.
Hivyo ameieleza jamii kuwa inapofuga sungura isilenge tu kwenye nyama yake bali mbolea na dawa.