Digrii Nyingine Ya Kichina, Kiswahili Kuanzishwa
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu Dar es Salaam (UDSM), kimeanzisha Digrii ya awali ya Elimu katika lugha ya Kichina na Kiingereza.
Aidha kipo katika mpango wa kuanzisha digrii nyingine itakayojikita katika masomo ya Kichina na Kiswahili.
Mkurugenzi wa Shahada ya Uzamili UDSM, Rose Upour amesema hayo alipomwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma chuoni hapo, Profesa Bonaventure Rutinwa kwenye Mashindano ya Awali ya Lugha ya Kichina Taasisi ya Confucios.
Upour amesema chuo hicho kinatoa stashahada katika lugha ya Kichina pamoja na kozi mbalimbali za muda mfupi katika lugha ya kichina.
“Hapa nchini wazungumzaji wa lugha ya kichina ni zaidi ya 200,000 na kuna makampuni zaidi ya 500 yanayoendesha shughuli zake hapa nchini.
” Hivyo kujifunza kichina kutakuwa na manufaa makubwa kwa wajifunzaji na kufanya hivyokutawaongezea fursa ya ajira na hatimaye kupata kipato,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi hiyo ya kichina, Dkt. Musa Hans amesema tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2002, yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa awamu mbili.
“Awamu ya kwanza ni mashindano ya awali katika nchi mbalimbali duniani, awamu ya pili ni mashindano ya bara na fainali ya dunia ambayo hufanyika China,” amesema.
Amesema zaidi ya wanafunzi milioni 1.5 kutoka zaidi ya nchi 150 wameshiriki mashindano hayo ya awali na kuonesha mafanikio katika kujifunza kichina.
Amesema zaidi ya washiriki 5000 wamekwenda China kushiriki katika mashindano ya mabara na fainali ya dunia.
” Lengo la mashindano haya ni kuwapa jukwaa vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani kuonesha ujuzi wao wa lugha ya kichina, kukuza mawasiliano baina yao, na kuwahamasisha kukifunza lugha ya kichina,” amesema.
Dkt. Hans amesema kwenye mashindano hayo walishiriki wanafunzi 16 waliotoka UDSM, Chuo cha Uhusiano wa Kidiplomasia, na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Washindi watashiriki katika mashindano yatakayofanyika Mei, chuoni hapo.
Naye Mwambata wa Masuala ya Utamaduni kutoka Ubalozi wa China nchini Tanzania, Xu Yongilang amesema zaidi ya nchi 180 duniani zinafundisha lugha ya Kichina.
Amesema karibu watu milioni 200 nje ya China wanajifunza lugha hiyo.
“Tunatarajia wanafunzi waendelee kujifunza kwa bidii, walimu wazidi kung’ara na jamii iendelee kuiunga mkono Taasisi ya Confucius,” amesema.
Mwanafunzi anayejifunza lugha ya kichina UDSM, Neema Joines amesema ameanza kujifunza tokea akiwa kidato cha kwanza, na kwamba lugha hiyo inawawezesha kupata kazi, marafiki hivyo wazazi wasiwazuie watoto wao kusoma lugha hiyo.
Naye mwanafunzi mwingine anayesoma lugha hiyo chuoni hapo, Aisha Yahya amesema kuzungumza lugha ya kichina na kumpa fursa ya kushiriki mashindano hayo kunamwongezea ujasiri.