Na Lucy Ngowi
DODOMA: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetafiti suluhisho la kielimu na utafiti kuhakikisha nyuki wadogo hawapotei kwa kuwa moja ya kazi wanayoifanya ni uchavushaji wa mimea mbalimbali.
Mwanasayansi wa nyuki kutoka UDSM, Gabriel Mwambogela amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Habari kuhusu suluhisho hilo.

Amesema njia mojawapo ya kuhakikisha nyuki hao wadogo wanaendelea kuwepo ni kubaini maeneo wanapopatikana na kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu umuhimu wao.
Amesema nyuki wadogo hawa wana uwezo wa kuchavusha maua yenye saizi tofauti tofauti, jambo linalosaidia katika kuongeza wingi na utofauti wa mazao.
“Aidha, asali inayotokana na nyuki hawa ina virutubisho vingi na hutumika kama tiba katika maeneo mbalimbali.
“Katika baadhi ya maeneo nchini, jamii imekuwa ikiwachukulia nyuki hawa kama wa laana kwa imani kuwa asali yao husababisha kuharisha au kutoa mimba,” amesema.
Ameongeza kuwa, baada ya kupewa elimu, mitazamo hiyo imebadilika na jamii sasa imeanza kuwaacha nyuki hao waendelee kuchangia kwenye mfumo wa ikolojia.
Amesena Ulimwenguni kuna aina 605 za nyuki wadogo, huku Afrika Bara ikiwa na aina 33. Tanzania ina jumla ya aina 12, ambazo zote zina mchango mkubwa katika uchavushaji wa mimea.
Ripoti ya utafiti huo imeonyesha kuwa maeneo ya ukanda wa mashariki mwa Tanzania yana idadi kubwa ya nyuki wadogo.
Amesema kupitia elimu na uhamasishaji, watafiti wa UDSM wanasisitiza umuhimu wa kuwalinda wadudu hao kwa mustakabali wa usalama wa chakula na mazingira.