Na Lucy Ngowi
DODOMA: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeanzisha teknolojia mpya kupitia programu ya simu janja inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kilimo kwa wakulima nchini.
Mhadhiri Msaidizi wa UDSM katika Idara ya Uhandisi wa Kilimo, Vicent Tsoray amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa na Kimataifa mkoani Dodoma.

Amesema Programu hiyo imeundwa kwa mfumo wa kipekee wenye sehemu mbili kuu moja kwa ajili ya wakulima na nyingine kwa watoa huduma wa kilimo.
Amesema Watumiaji wataweza kujisajili kama wakulima au watoa huduma kwa kuweka taarifa zao muhimu kama majina na nywila, ili kupata ufikiaji kamili wa huduma zilizopo kwenye programu hiyo.
“Kupitia APP hiyo, mkulima ataweza kuchagua huduma anayohitaji iwe ni upatikanaji wa mashine za kilimo kama matrekta, mashine za kuvunia, vifaa vya kunyunyizia dawa au kusambaza mbolea na kuainisha ukubwa wa shamba pamoja na aina ya mazao anayolima.
“Mfumo utamuonyesha orodha ya watoa huduma waliopo, na mkulima ataweza kuchagua mmoja kulingana na mahitaji yake,” amesema.
Amesema mtoa huduma atakapopokea ombi hilo, mfumo utaelekeza hatua kwa hatua jinsi huduma itakavyotolewa hadi kukamilika.
Teknolojia hii inalenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na muda wa upatikanaji wa huduma za kilimo, na hivyo kuinua tija ya wakulima wadogo na wa kati.