Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimesaini mikataba na kampuni tatu za kichina ikiwemo KZJ Newa Materials Group Co. Ltd, Ju Ye Concrete Co. Ltd na CRJE (East Afrika) Ltd, lengo likiwa ni kuongezea maarifa ya vitendo wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema hayo wakati wa utiaji saini na kampuni hizo chuoni hapo.
Amesema chuo hicho kimekuwa na utaratibu wa kushirikiana na kampuni ambazo zinaajiri wahitimu waliozalishwa na chuo hicho kwa lengo la kuwaongezea uzoefu katika kazi na maarifa zaidi.
“Leo tumesaini mikataba na kampuni za kichina kwa ajili ya kutoa nafasi za kufanya kazi kwa vitendo pamoja na kuwafadhili wanafunzi wanaosoma shahada za awali na uzamili chuoni hapa,”amesema.
Kuhusu teknolojia mpya ya uchanganyaji wa zege kwa moja ya kampuni waliosaini nao mkataba, Profesa Anangisye amesema wao kama chuo wanawaandaa wahandisi, hivyo teknolojia hiyo itawaongezea ujuzi na kwamba UDSM kinaweza kuwa ni chuo cha kwanza kupeleka teknolojia hiyo katika nchi nyingine za Afrika.
“Jukwaa hili linaonyesha dhamira yetu isiyoyumba katika malengo ya Dira ya 2061 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ina malengo hayo kusisitiza ubora wa utafiti, ushirikiano wa viwanda, na athari ya maana ya kijamii.
“Hatuoni ushirikiano huu kama tu ushirikiano rasmi, lakini kama uwezeshaji wa kimkakati utafiti, maendeleo ya ujuzi na teknolojia ambao ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Zege ya Ju Ye, Xu Hongjuani amesema uzinduzi huo ni wa kikao cha kwanza cha ushirikiano wa uchanganyaji wa zege.
Amesema kampuni hiyo imekuwa na washirika muhimu katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo daraja la Magufuli, daraja la Tanzanite, Uwanja wa Ndege Dodoma na miundombinu mingine mbalimbali.