NA Danson Kaijage
DODOMA:WAUMINI wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kuwaombea dua njema kwa Mungu Marais, Samia Suluhu Hassan na Hussein Ali Mwinyi ili uongozi wao uendelee kuwa wa amani na utulivu.
Katibu wa Sekretarieti Baraza la Ulamaa Taifa na Mratibu Ofisi ya Mufti Makao Makuu- Dodoma,Sheikh Swed Twaibu Swed amewataka waumini hao kuomba dua hiyo, alipokuwa akizungumza na umati wa waumini wa Dini ya Kiislamu katika uwanja wa mpira wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Amesema dini ya Kiislamu inaelekeza kuwa kila siku ya Ibada ya Ijumaa kuna dua ya kumwombea kiongozi mkuu ambaye ni Rais
Amesema maombi ya kuwaombea marais hao ni muhimu kwani wanaongoza uhai wa watu kwa mamlaka waliyonayo duniani, hivyo ni lazima wawe na mguvu ya Mwenyezi Mungu ya kuwaongoza kufanya mambo ambayo yana busara,hekima,upendo na kudumisha amani sambamba na kuendeleza Muungano uliopo.
Sheikh Swed amesema wakati waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa katika mfungo Mtukufu wa Ramadhani walikuwa wakimcha Mungu kwa bidii, sasa wamemaliza kwa kuisherekea Eid ul-Fitr wanatakiwa kuwa na nguvu ile ile ya maombi kama ilivyo katika kipindi cha Ramadhani.
“Mnaweza kuona kuwaombea viongozi hususani Rais ni jambo la kawaida, ni muhimu kufanya maombi ili Kiongozi mkubwa wa nchi kama vile Rais Samia awe na afya njema.
” Azidi kusimamia misingi ya utu na haki sambamba na kufanya kazi kwa masilahi mapana ya watu anaowaongoza badala ya kuwaza kujinufaisha,” amesema.
Amesema baada ya kumaliza mfungo, mtukufu wa Ramadhan, waumini wanatakiwa kuonesha mabadiliko ya nguvu ya maombi kitabia,kiuchumi na kwa mwenendo mzima wa maisha.
Pia amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.