Awajulia Hali Majeruhi 16, Waliopoteza Maisha 11
Na Lucy Ngowi
KAGERA: WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeanza kufanyia kazi maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya marekebisho ya kuwa na mfumo wa leseni za udereva ili kuwapunguzia alama madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama barabarani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema hayo baada ya kufika eneo la Kabukome katika Kata ya Nyarubango wilayani Biharamulo mkoani Kagera, kulipotokea ajali ya basi la abiria lenye namba za usajili T857 DHW.

Pia aliwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupewa matibabu katika Hospitali Teule ya Biharamulo, Disemba 21, 2024.
Bashungwa amesema maelekezo hayo ya Rais Samia ni pamoja na kuwafungia leseni madereva wanaofanya makosa yanayohatarisha usalama barabarani.
Basi hilo lililopata ajali lilikuwa linafanya safari kutoka Kigoma kwenda Bukoba wakati liliposimama kushusha abiria ambaye alipitilizwa kwenye kituo, lilishindwa kuondoka na kurudi nyuma kisha kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo imesababisha vifo vya abiria 11 na majeruhi 16 ambapo majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali Teule ya Biharamulo mkoani Kagera.
Bashungwa ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na ajali hiyo na kutoa wito kwa watanzania kuendelea kuwaombea majeruhi wapone haraka.
Kwa Upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo majeruhi waliko, Gresmus Sebuyoya amesema majeruhi 26 wameruhusiwa na wengine 16 wanaendelea na matibabu na ungalizi wa karibu.
“Tumebaki na watoto wanne ambao wanaendelea vizuri, wanaume tunao sita, vifo tulikuwa navyo 11, wanawake watano, wanaume wanne na watoto wawili” amesema.