Na Lucy Ngowi
DODOMA: TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imewataka wananchi na vyama vya umwagiliaji kufuata masharti ya kisheria katika matumizi ya rasilimali za umwagiliaji, kwa kuwa kuna makatazo yaliyoainishwa kisheria yanayolenga kulinda mazingira na kuongeza tija katika kilimo nchini.
Wakili wa Serikali kutoka Tume hiyo, Baraka Chipamba, amesema hayo katika maonesho ya wakulima ya Kitaifa yanayoendelea mkoani Dodoma,
Amesema Sheria ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Na. 4 ya mwaka 2013, iliyotokana na Sera ya Umwagiliaji ya mwaka 2010, imeweka masharti madhubuti kwa ajili ya kusimamia shughuli za umwagiliaji nchini.
“Sheria hii imeweka makatazo muhimu kama uvamizi wa maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya kemikali katika vyanzo vya umwagiliaji, uvuvi bila kibali katika maeneo hayo, na uchepushaji wa maji kinyume na utaratibu,” amesema Chipamba.
Amesema makatazo hayo yanahitajika kuzingatiwa kwa sababu uvunjaji wake unaathiri moja kwa moja tija ya kilimo na uhifadhi wa mazingira.
Aidha, ameviomba vyama vya umwagiliaji ambavyo vina nafasi kubwa katika utekelezaji wa sheria hiyo, kusaidia kutoa elimu kwa wanachama wao na kuhakikisha taratibu zinafuatwa.
“Kuna watu wanajitokeza na kuingilia skimu za umwagiliaji bila kuwa sehemu ya mradi, wanachepusha maji au wanafanya uvuvi bila kibali hii ni kinyume cha sheria,” amesema.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Tume hiyo, Vicky Mbunde, amesema jukumu kuu la Tume ya Kurekebisha Sheria ni kufanya mapitio ya sheria zilizopo ili kuhakikisha zinaendana na wakati na mazingira ya sasa, pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa umma.
Amesema Tume hufanya tafiti za kisheria ili kubaini kama sheria fulani bado inafaa kwa mazingira ya sasa au ina upungufu unaohitaji kurekebishwa. Kazi hiyo hufanyika kwa kushirikisha wananchi moja kwa moja.
“Sisi hatupendekezi sheria kutoka kichwani, tunashirikiana na wananchi. Tunataka kusikia wanasema nini kuhusu sheria zilizopo – ndipo tunapata maoni halisi ya kile kinachohitaji kuboreshwa,” alisema Mbunde.
Pia alieleza kuwa Tume hushiriki kwenye maonyesho mbalimbali ya kitaifa ili kuwafikia wananchi na kuwaelimisha juu ya mchakato wa maboresho ya sheria na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika mabadiliko hayo.