Mwinyi: Serikali ipo tayari kushirikiana nao katika kila hatua
Na Lucy Ngowi
ARUSHA: KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Ahmed Mwinyi amepongeza Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa kuwekeza kitega uchumi katika mkoa huo, akisema hatua hiyo ni ya kuungwa mkono na kuigwa.

Mwinyi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru ametoa pongezi hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo, mkoani Arusha.
Pia amepongeza shirikisho hilo kwa kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, kushiriki tukio hilo muhimu.

“Serikali ya Mkoa wa Arusha itaendelea kushirikiana kwa karibu na TUCTA katika kuhakikisha kwamba kila hatua wanayochukua ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na maendeleo ya kijamii, inafanikiwa. Tutaendelea kuwaunga mkono katika kila jambo watakalolihitaji,” amesema.
Pia Mwinyi amelipongeza shirikisho hilo kwa hatua kubwa za maendeleo linazoendelea kuzifanya, zikiwemo mageuzi na mapinduzi chanya katika usimamizi wa rasilimali zake pamoja na nia ya dhati ya kukuza maendeleo ya wananchi kupitia vitega uchumi kama jengo hilo.

“Tunatambua mchango mkubwa wa TUCTA siyo tu kwa wafanyakazi, bali pia kwa maendeleo ya jamii. Uwekezaji huu siyo tu unaongeza thamani ya ardhi na mandhari ya jiji la Arusha, bali pia ni sehemu ya ajira na mapato kwa wakazi wa eneo hili,” amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na shirikisho hilo katika kuhakikisha kila mpango na shughuli zao zinafanikiwa kwa manufaa ya taifa.
