Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, ameitaka Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TSLB) kuimarisha huduma zake kwa njia za kisasa za kidijitali.
Dkt. Onar amesema katika kukabiliana na changamoto za elimu ya karne ya 21, ni muhimu kwa TSLB kutumia teknolojia ya kisasa kama maktaba mtandao, mifumo ya rejea ya kidijitali, na huduma bunifu kama “Maktaba Kiganjani” ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

“Maktaba zetu hazipaswi kuwa maeneo ya vitabu tu, bali vituo vya maarifa yanayopatikana kwa urahisi, haraka, na bila vikwazo vya kijiografia au kijamii,” amesema.
Amesema maktaba zina mchango mkubwa katika kukuza usawa wa kielimu, na hivyo ni lazima kila mwananchi apate fursa sawa ya kusoma na kujifunza.
Amesema TSLB inapaswa kuendeleza utamaduni wa kusoma vitabu miongoni mwa wananchi wa rika na makundi yote, ikiwa ni pamoja na watoto, vijana, na watu wazima.

Vituo vya malezi vilivyopo katika baadhi ya maktaba pia vilisifiwa kwa kusaidia watoto kusoma na kucheza katika mazingira rafiki ya kujifunzia, jambo linalowajengea msingi bora wa elimu ya awali.
Katika nyanja ya utafiti, Dkt. Hussein amehimiza umuhimu wa kuhifadhi nyaraka za kihistoria na kutoa taarifa sahihi kwa wanafunzi na watafiti kupitia mifumo bora ya rejista za kitaaluma.