Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imetunukiwa tuzo ya mshindi wa kwanza kutokanana mchango wake kiuchumi na kijamii.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa tuzo hizo kwa Taasisi zilizoonyesha juhudi katika kuwapatia jamii maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo, TPHPA imeonyesha ufanisi wa hali ya juu katika kudhibiti balaa la panya.

Taarifa inasema TPHPA imedhibiti baa la panya katika mikoa 16, wilaya 54, kata 540, na vijiji 1,395.
“Juhudi hizi zimesaidia wakulima wapatao 58,886 kwa kuokoa jumla ya ekari 895 za mazao yao, hivyo kuimarisha usalama wa chakula na kuleta athari chanya kwa uchumi wa nchi.
“Pia TPHPA ilifanya kazi kubwa katika kudhibiti ndege aina ya kwelea kwelea. Zaidi ya ndege milioni 80 waliovamia mazao katika halmashauri 24 walikabiliwa vilivyo,” imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo udhibiti huo umewezesha wakulima kuokoa takriban tani 100,000 za nafaka, ikiwa ni pamoja na mpunga, uwele, na mtama, hivyo kuondoa hatari kubwa ya upungufu wa chakula.
Katika tukio hilo, Mamlaka iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Profesa Andrew Temu, na Mkurugenzi Mkuu, Profesa Joseph Ndunguru, ambao walipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mamlaka.
“Tuzo hii sio tu inatambua mafanikio ya TPHPA bali pia inasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika kufikia malengo ya pamoja.
“Kwa kupokea tuzo hii, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania imejidhihirisha kama mfano wa kuigwa katika juhudi za kuboresha maisha ya wananchi na kuendeleza uchumi wa nchi,” imesema taarifa hiyo.