Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NDEGE itakayotumika kudhibiti milipuko ya kwelea kwelea na nzige kwenye mashamba ya wakulima, inatarajiwa kuwasili nchini Tanzania muda wowote kuanzia sasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mmea na Viuatilifu (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Gazeti la Mfanyakazi Tanzania.
Profesa Ndunguru amesema ndege hiyo ya TPHPA, imenunuliwa na serikali Sh. Bilioni sita, ipo katika hatua za mwisho za matengenezo.
Amesema marubani wa kurusha ndege hiyo kutoka TPHPA wapo nchini Marekani kwa ajili ya mafunzo.
“Hii ndege itaenda kuleta tija kubwa sana kwenye udhibiti wa visumbufu kama vile ndege aina ya kwelea kwelea na nzige kwenye mashamba ya nafaka,
“Kwa hiyo badala ya sisi kutegemea ndege ya kukodi kutoka Shirika la Nzige Nairobi sasa ikitokea tu mlipuko tutakuwa tunatumia ndege yetu.
“Na bado Tuna mpango wa kununua ndege nyingine,” amesema.