Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imezindua rasmi kifaa kipya cha kisasa aina ya MinION, chenye uwezo wa kutambua vinasaba vya wadudu, mimea, na magonjwa moja kwa moja shambani,
Teknolojia ambayo kwa mara ya kwanza upande wa kilimo inatumiwa Afrika na Tanzania ikiwa kinara.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo katika maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa na Kimataifa yanayofanyika mkoani Dodoma.
Amesema kifaa hicho ni mkombozi mkubwa kwa sekta ya kilimo nchini na kimethibitishwa kuwa na uwezo wa kutumika kwa mafanikio katika mazingira ya shamba.

Amesema kifaa hicho ambacho ni kidogo, kinaweza kutoa majibu ya uchunguzi ndani ya dakika 20, kinatarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kusaidia wakulima kupata majibu ya haraka kuhusu visumbufu vya mimea, hivyo kuwezesha matumizi sahihi ya viuatilifu na kuongeza tija ya uzalishaji.
“Kifaa hiki kilibuniwa Uingereza kwa ajili ya kutambua virusi vya Zika na Ebola, lakini sisi Tanzania tumefanya majaribio ya kina na tumethibitisha asilimia 100 uwezo wake katika kubaini visumbufu vya mimea, wadudu na magonjwa.
“Sasa kinatumiwa kwa mara ya kwanza Afrika hapa nchini kwetu,” amesema.
Amesema kupitia ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Chakula Duniani (FAO), na Serikali ya Tanzania, TPHPA imefanikiwa kupata vifaa 20 vya MinION ambavyo vitasambazwa kwenye vituo vya mamlaka hiyo katika kanda mbalimbali nchini.

Amesema lengo ni kuwezesha uchunguzi wa kisayansi wa wadudu, magonjwa na mimea sugu kwa haraka, katika maeneo yote ya Tanzania.
Ndunguru amebainisha kuwa teknolojia hiyo pia itasaidia kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania kwenye soko la kimataifa kwa kuwa sasa nchi itakuwa na uwezo wa kuthibitisha ubora wa mazao kwa haraka, kabla ya kuuza nje ya nchi.

“Hili ni jicho la kisayansi ambalo litazuia uingizwaji wa bidhaa zilizo na magonjwa hatari, na pia kusaidia kwenye utambuzi wa mimea, viumbe wa majini, wanyamapori na hata magonjwa ya binadamu,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya ya Mimea kutoka TPHPA, Dkt. Begnius Ngowi, amesema kifaa hicho kitaondoa ucheleweshaji wa majibu ya maabara na kukomesha utumiaji wa viuatilifu kwa kubahatisha.
“Changamoto kubwa imekuwa wakulima kutambua aina ya mdudu au ugonjwa kwa macho tu, na matokeo yake wanatumia dawa isiyofaa.

“Kwa mfano, mdudu Tuta absoluta maarufu kwa jina la ‘Kantangaze’ huonekana kama mdudu mwingine wa kawaida, lakini dawa zake ni tofauti kabisa,” amesema.
Amesema kupitia kifaa hicho, wataalamu wataweza kufanya uchunguzi wa kitaalamu hapo hapo shambani na kumpa mkulima suluhisho sahihi bila kuchelewa.

Baada ya maonesho hayo, wataalamu kutoka TPHPA wanatarajia kuanza kambi ya uchunguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoa wa Iringa, maarufu kwa kilimo cha mbogamboga na matunda, ili kubaini chanzo cha changamoto zinazowakabili wakulima wa eneo hilo.
