Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), imekusanya zaidi ya sampuli 10,000 za mbegu za asili, kwa ajili ya kuzihifadhi na kuzifanyia utafiti ili kujua uwezo na sifa ilizonazo.
Mkuu wa Kitengo cha Taifa cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea kutoka TPHPA, Mujuni Sospeter amesema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.
Amesema, ” Mamlaka inafanya utafiti kujua sifa zake za awali, kujua zina uwezo gani na baada ya kujua huo uwezo inatusaidia kuweza kushirikiana na taasisi hasa za utafiti ili wazitumie kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora zaidi,”.
Amesema msingi wa utafiti unatokana na mbegu hizo za asili, ambapo kwa kutumia sifa za mbegu hizo watafiti wana nafasi ya kutengeneza mbegu bora zaidi.
“Kwa tafiti ambazo tumezifanya zinaonyesha hizi mbegu za asili zina sifa mbalimbali nyingi tu muhimu, virutubisho vingi tu muhimu ambazo hatuhitaji kuzipoteza,” amesema.