Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Afya ya Mmea na Viuatilifu (TPHPA), inatarajia kuwa na ndege nyuki 41 (drones), baada ya kukamilisha ununuzi wa 20, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za kudhibiti visumbufu vya mazao.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi Tanzania, alipokuwa akielezea mafanikio ya mamlaka hiyo mpaka sasa.
Profesa Ndunguru amesema,”Tuna drones 21 lakini tayari sasa hivi tuko kwenye hatua ya mwisho ya kukamilisha drones nyingine 20, hivyo tutakuwa nazo 41,”.
Amesema wamekuwa wakitumia ndege nyuki hizo pamoja na vifaa vya kisasa kufanyia uchunguzi wa visumbufu, kufuatilia ili kuvidhibiti kabla havijaleta madhara kwa wakulima.
Amesisitiza kuwa kwa upande wa vitendea kazi mamlaka imejiimarisha.
“Kwa maana ya magari, kompyuta na pikipiki za kufanyia ukaguzi. Mwaka jana 2024 tulipewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) magari nane, pikipiki 39,
“Lakini na sisi tumenunua mwaka huu wa fedha 2024/2025, magari 10, pikipiki 39 kwa kutumia fedha zetu za ndani kwa hiyo hicho sio kitu kidogo,” amesema.