Na Lucy Ngowi
WANANCHI wametakiwa kujenga utamaduni wa kutoa taarifa mapema, pindi wanapoona ndege aina ya kwelea kwelea au wadudu waharibifu nzige au viwavijeshi vamizi wameingia shambani ili zichukuliwe hatua haraka za kuwadhibiti kabla ya kufanya uharibifu wa chakula.
Hayo yameelezwa na Ofisa kutoka Mamlaka ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA), Godlove Kirimbo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea jijini Dodoma.
Amesema wananchi wanapoona visumbufu hivyo ,watoe taarifa kwa halmashauri husika ambayo pia itatoa taarifa kwenye Mamlaka hiyo kisha hatua za kuwadhibiti zinafuata .
Amevitaja visumbufu hivyo vya mlipuko kuwa ni ndege aina ya kwelea kwelea, panya waharibufu wa mazao, nzige na viwavijeshi kwamba hutokea kwa ghafla vikiwa katika makundi makubwa na kusababisha uharibifu wa chakula ndani ya muda mfupi.
Kirimbo amesema kuanzia Februari mwaka huu, kulikuwa na mlipuko mkubwa wa kwelea kwelea kwenye halmashauri 24 nchini ambapo zaidi ya kwelea kwelea milioni 70 walivamia na kushambulia mazao ya nafaka mtama,uwele,mpunga na alizeti.
“Mwaka huu tumerekodi kwelea kwelea zaidi ya milioni 70 walikuwa Tanzania na kundi sogo la kweleakwelea lenye milioni moja linaweza kuharibu tani 25 kwa siku moja,
“Lakini kundi dogo la nzige milioni 40 linaweza kuharibu chakula ambacho kingeweza kuliwa na watu 35,000 kwa siku,kwa hiyo unaona kwamba viumbe hivi wakiachwa ,nchi itaingia kwenye baa kubwa la njaa,” amesema.
Amesema visumbufu vya mlipuko ni hatari kwa usalama wa chakula nchini huku akisema TPHPA wana jukumu la kuhakikisha usalama wa chakula nchini unalindwa kwa kuvidhibiti visumbufu hivyo.
Kwa mujibu wa Kirimbo,visumbufu aina ya kweleakwelea ni hatari kwa usalama wa chakula kwa sababu wana tabia ya kuishi kwenye makundi makubwa ya kuanzia milioni moja kuendelea.