Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), wamesaini hati ya makubaliano na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), katika maeneo mbali mbali likiwemo la udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao,
Akizungumza mara baada ya kusaini hati hiyo ya makubaliano, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema kuwa moja ya eneo la ushirikiano ni kwa kuwa kuna sayansi katika chuo hicho sawasawa na shughuli zinazofanyika katika mamlaka yake.
Amesema watashirikiana na chuo hicho kufanya utafiti na kutumia matokeo ya utafiti ili kutoa suluhu kwa wakulima katika maeneo ya magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao.
“Ushirikiano huu utawezesha kufanya kazi pamoja na kuja na suluhu. Tunataka kutumia ushirikiano huu kujengeana uwezo hasa katika kuandika miradi ikiwa ni mkakati mojawapo wa kutafuta fedha kuendesha majukumu ya kila siku.
“Kuna umuhimu wa kushirikiana sisi kwa sisi,” amesema Profesa Ndunguru.
Profesa Ndunguru amesema mamlaka yake ina vifaa vya kisasa kwenye maabara na ambavyo ni vingi hivyo wanafunzi wa MUCE wanaweza kwenda na kufanya majaribio kwa vitendo, ili wajue utafiti wanaoufanya unapaswa kutoa suluhu kwa jamii.
Ametaja ushirikiano mwingine utakuwepo katika kuandaa mikutano ya pamoja ambayo itawaweka wadau pamoja kwa ajili ya kupeana taarifa, kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali zinazofanyiwa utafiti na wataalam wa MUCE na TPHPA.
Amesema pia mamlaka yake itawasimamia wanafunzi wa MUCE wanaosoma shahada ya uzamili na uzamivu kwa ajili ya kutoa mafunzo mbalimbali.
Amemalizia kwa kusema mamlaka hiyo imeanzisha program ambayo wanataka kijana atakayekuwa na ubunifu utakaosaidia kutambua magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao, ubunifu huo utafadhiliwa na TPHPA.