– Biteko Mgeni Rasmi
Na Danson Kaijage
DODOMA: TIMU zitakazoshiriki michezo mbalimbali katika Bonanza la Wizara ya Nishati na taasisi zake zimeshawasili Dodoma.
Katika bonanza hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt..Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Neema Mbuja amesema hayo alipozungumza na wanahabari kuhusu bonanza hilo litafanyika kesho Juni 28, 2025 katika Viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma.
Ameitaja michezo itakayoshindaniwa katikq bonanza hiyo kuwa ni Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Mpira wa Kikapu, Kuvuta Kamba, michezo ya jadi ikiwemo bao, drafti na kufukuza kuku.
‘’ Nipende kuchukua fursa hii kuzikaribisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kushiriki kikamilifu bonanza ambalo linaleta fursa ya kufahamiana na kubadilishana mawazo baada ya muda wa kazi pamoja na kufanya mazoezi ili kujenga afya,” amesema.
Ametaja kauli mbiu ya bonanza hilo ni, ‘Michezo kwa Afya bora, Shiriki uchaguzi 2025’ ikiwa na lengo pia la kuhamasisha wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 .
Mbuja amezitaja taasisi zitakazoshiriki kuwa ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu Petroli ( PURA).
Nyingine ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania ( TGDC), Kampuniya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishajina Usambazaji wa Umeme (ETDCO).
Pia Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo za Zege ( TCPM), Kituo cha kuuzia mafuta ya petrol na dizeli cha Serikali (TANOIL), Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA).
Amesema bonanza hilo ni la pili kufanyika tangu kuasisiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko mwaka jana.