Dodoma: KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetaja mambo 10 ya msingi ambayo yamesababisha kituo hicho kupaa kiuchumi Barani Afrika ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Gilead Teri akitoa taarifa ya utekelezaji wa mafanikio ya kituo hicho kwa miaka minne, amesema njia pekee iliyofanikisha mafanikio makubwa ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa sekta binafsi hususani wazawa.
Jambo lingine ambalo ameeleza kuwa limechangia maendeleo na mafanikio katika kituo hicho ni pamoja na ubadilishaji wa sheria ya uwekezaji ambayo ni sheria ya uwekezaji na maboresho ya ubia binafsi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji Teri amesema kuwa mtanzania mwenye kukidhi vigezo vya uwekezaji na mwenye mtaji wa Sh. Mil. 100 anatambuliwa na kupewa sifa ya uwekezaji.
Amesema kuwa mtanzania mwenye taarifa ya benki yenye kiasi cha Sh. Milioni 10 benki kwa miezi mitatu hadi sita kwa kuonesha mzunguko wa kutoka na kuingia anapewa sifa na kuwa na kigezo cha kuwekeza.
Ameyataja mafanikio mengine ya TIC kuwa ni maboresho ya kuwahudumia watanzania kwa kuongeza weledi pamoja na kuongeza makusanyo ya kila mwezi kutola Sh, Milioni 400 kwa mwezi mwaka 2022 na kufikia Sh. Bilioni moja kwa mwezi kwa mwaka 2024 na kufanikiwa kukusanya Sh. Bilioni 12 kwa mwaka 2024.
Akizungumzia fanikio la nne Teri amesema ni kukuza diplomasia ya uchumi na kufanyika ziara za kimkakati zinazoshawishi uwekezaji wa watu kutoka katika mataifa mbalimbali na balozi zote 44 kufanya changamfu kwa kuwavutia wawekezaji nchini.
Pia amesema kuwa kumekuwepo na ongezeko la mtaji,viwanda na ajira pamoja na kuongezeka kwa teknolojia sambamba na uwekezaji kwenda Mikoa yote ya Tanzania pia kumekuwepo na ongezeko la wawekezaji mahiri na muhimu,kuongezeka kwa wawekezaji wa ndani na kuwepo kwa uwekezaji mtambuka nchini tofauti na nchi nyingine Duniani.