Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Elimu Tanzania(TEN/MET), pamoja na Kituo cha Sheria za Haki za Binadam (LHRC), unashauri kuwekwa kwa vifungu vya sheria vinavyopiga marufuku matumizi ya viboko shuleni na adhabu nyinginezo zinazoathiri utu wa mtoto.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji LHRC, Fulgence Massawe ametoa ushauri huo leo Machi 11, 2025 wakati wakizungumza na Waandishi wa Habari juu ya matukio ya kujeruhiwa na kuuawa kwa wanafunzi kutokana na adhabu kali ya viboko mashuleni.
Amesema, “Tunashauri kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na mapitio yake. Marekebisho haya yataimarisha mfumo wa ulinzi na usalama wa wanafunzi na kuondoa mianya ya matumizi mabayaya mamlaka ya nguvu dhidi ya wanafunzi, hatua ambayo itasaidia kuzuia vitendo vya ukatili ndani na nje ya shule,”.
Amesema wanaiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itoe waraka rasmi unaoelezea walimu wote kuacha matumizi ya adhabu za viboko na kuelezea mbinu mbadala za nidhamu zinazolinda utu na haki ya watoto, wakati mchakato wa marekebisho ya sheria ya elimu ukiendelea.
Pia wameshauri serikali kuendelea kuimarisha utekelezaji wa kuanzishwa madawati ya ulinzi na usalama kwenye shule zote ifikapo mwaka 2029.
“Madawati haya yanatoa mfumo rasmi wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya watoto wanaokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali shuleni,” amesema.
Pia wameshauri hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na tukio hilo lakikatili na matukio mengine yanayofanna na hilo, ambapo yamevunja haki ya msingi ya mtoto ya kuishi, kinyume na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Naye Mratibu Kitaifa TEN/MET Martha Makala amesema Februari 26, 2025 ziliripotiwa taarifa kupitia vyombo vya habari za kufariki kwa mwanafunzi aitwae Mhoja Maduhu wa Kidato cha pili aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari Mwasama iliyopo Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
“LHRT na Mtandao wa Elimu Tanzania tunasikitishwa sana na tukio hili, ambalo si tu linakiuka haki za mtoto,bali pia linakwenda kinyume na sheria na miongozo ya elimunchini,” amesema.