Na Mwandishi Wetu
GEITA: Tanzania inaendelea kutekeleza vigezo vya kimataifa vya Asasi ya EITI kwa kiwango cha kuridhisha, sambamba na Sheria ya TEITA ya mwaka 2015.
Meneja wa Kitengo cha Uwazi na Uwajibikaji kutoka Taasisi ya Uangalizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Erick Ketagory, amesema hayo katika Maonesho ya Nane ya Sekta ya Madini.
Amesema tangu kujiunga na Mpango wa Kimataifa unaolenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji (EITI) mwaka 2009, TEITI imetoa jumla ya ripoti 15 za ulinganishi wa malipo kati ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia na mapato ya serikali.
“Ripoti ya hivi karibuni, ya mwaka 2022/2023, ilitolewa Juni 30, 2025,” amesema.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa takwa la kuweka wazi mikataba ya serikali na kampuni katika sekta ya uziduaji umeanza rasmi, na mikataba hiyo sasa inapatikana kupitia tovuti ya TEITI.
Ketagory ametoa wito kwa wananchi wa Geita kutembelea banda la TEITI ili kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya taasisi hiyo na namna ya kutumia taarifa na takwimu zinazopatikana kwenye ripoti zake.
Taarifa na ripoti zote za TEITI zinapatikana kupitia tovuti rasmi: www.teiti.go.tz
TEITI imeshiriki katika Maonesho ya Nane ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji.
Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi Septemba 22, 2025 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.