Atugonza David akiwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Pangale Mwalimu Sengi Msaru wakati wa kukagua mradi wa ukarabati wa maabara tatu za Sayansi zilizofadhiliwa na UNICEF, CANADA kwa usimamizi wa TEA.
Na Mwandishi Wetu
TABORA: MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Serikali ya Canada, wamekamilisha utekelezaji wa miradi 10 ya miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
Miradi hiyo, yenye thamani ya takriban Sh. Milioni 284, imetekelezwa katika shule sita kwa lengo la kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kufundishi, Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa maabara, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

Muonekano wa ndani wa maabara ya Sayansi shule ya Sekondari Pangale baada ya ukarabati uliofadhiliwa na UNICEF, Serikali ya CANADA na kuratibiwa na TEA
Akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Ofisa Miradi kutoka TEA, Atugonza David, amesema ujenzi umekamilika na miundombinu hiyo iko tayari kutumika.
“Tumemaliza maabara nane za sayansi katika shule nne, tumejenga matundu 10 ya vyoo katika shule moja na kukamilisha vyumba vinne vya madarasa katika shule nyingine,” amesema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kamagi, Mwalinu Merina Mbiha (kulia) akitoa maelezo kwa Atugonza David Ofisa Miradi kutoka TEA, alipofanya ziara ya kukagua ukarabati wa maabara mbili za Sayansi shuleni hapo
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ngulu, Mwalimu Israel Mwambikwa, amesema shule yake imenufaika na ujenzi wa maabara mbili, hatua iliyoongeza hamasa ya wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi, hasa kwa wasichana.
“Tuna jumla ya wanafunzi 666, nusu yao ni wasichana. Tangu kukamilika kwa maabara, wasichana wameanza kufanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi na idadi yao kwenye michepuo ya sayansi imeongezeka mara mbili,” amesema.

Baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Kamagi wakiwa nje ya maabara ya Kemia iliyokarabatiwa na UNICEF pamoja na Serikali ya CANADA kwa uratibu wa TEA
Mpango huu ni sehemu ya makubaliano kati ya TEA na UNICEF yanayolenga kuboresha fursa za elimu kwa watoto wote wa Kitanzania, kwa kuhakikisha mazingira salama na jumuishi ya kujifunzia.

Ofisa Miradi kutoka TEA Atugonza David akiwa na Mwalimu Mkuu shule ya msingi Kiloleli Mwalimu Festo Ponela (katikati) pamoja na mjumbe wa kamati ya shule Bw. Nicholaus Mbanka wakikagua ujenzi wa matundu 10 ya vyoo yaliyofadhiliwa na UNICEF, Serikali ya CANADA na kuratibiwa na TEA