Na Lucy Ngowi
GEITA: WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeeleza mpango wake wa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi katika siku za karibuni. hivyo umewakaribisha wawekezaji kushirikiana nao kwa mfumo wa ubia katika miradi hiyo ya kimkakati.
Ofisa Habari wa TBA, Adam Mwingira,amemweleza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati alipotembelea banda hilo katila maonesho ya nane ya sekta ya madini yanayomalizika leo Septemba, 28 mwaka huu 2025.

Mwingira amesema TBA imepanga kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa hivi karibuni na inakaribisha sekta binafsi kushiriki katika miradi hiyo kupitia ubia, hatua ambayo inalenga kuongeza kasi ya maendeleo ya miundombinu nchini.
Ameeleza miradi hiyo inatekelezwa maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa ya Geita na Chato ambapo TBA tayari imekamilisha na inaendelea na miradi mingine.
“Tunawakaribisha wawekezaji kushirikiana nasi kwa kuwa tunaamini ubia kati ya serikali na sekta binafsi utaharakisha utekelezaji wa miradi kwa ubora na kwa wakati,” amesema Mwingira.
Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kubadilisha sheria ya Majengo GN. Na. 595 ya mwaka 2023, inayoruhusu ushirikiano huo.
Amesema TBA inatekeleza miradi hiyo kwa kushirikiana na taasisi za kifedha pamoja na sekta binafsi. Miongoni mwa miradi iliyotajwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato, Hospitali ya Mkoa wa Geita, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ofisi ya TANESCO, na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.