Na Mwandishi Wetu
Wananch Wakaribishwa Kula NyamaPori Ya Kuchoma Sabasaba
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imesema serikali imeendelea kuimarisha mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta mbalimbali, hususan sekta ya utalii.

Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema hayo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere yajulikanayo kama Sabasaba mkoani Dar es Salaam.
Amesema kutokana na serikali kuimarisha mazingira hayo,
taasisi hiyo inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
“Tunawaambia Watanzania na wawekezaji wote kwa ujumla kuwa TAWA ni mahali sahihi kwa uwekezaji, unapotaka kuwekeza unakaribishwa sana.
“Ikumbukwe kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mazingira wezeshi Kwa wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi yetu,” amesema Maganja.
“Kama alivyofanya Mhe. Rais na sisi tunamuunga mkono Kwa kuhakikisha kwamba fursa hizi zinakuwa wazi Kwa wawekezaji wote na ndio maana tuko hapa kuwatangazia waje kuwekeza katika hii taasisi,” amesema.

Pia Maganja amesema TAWA inasimamia maeneo yenye rasilimali adimu, vivutio vya kipekee, na mandhari ya kuvutia ambayo yanatoa fursa kubwa ya uwekezaji endelevu kwa maslahi ya taifa na uhifadhi wa maliasili.
Ametaja baadhi ya maeneo yaliyo tayari kwa uwekezaji ni Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park (Arusha), Wami-Mbiki (Morogoro), Mpanga/Kipengere (Mbeya na Njombe), Tabora ZOO, Ruhila ZOO na maeneo mengine mengi yenye fursa mbalimbali.

Kwa upande wake, Ofisa Mhifadhi Mkuu kutoka TAWA, Dkt. Gladson Mlay amehamasisha wananchi kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho hayo, ambapo wanaweza kujionea wanyamapori hai wakiwemo simba, chui, fisi, mamba na spishi mbalimbali za ndege.
Pia amewaalika wananchi kuonja na kununua kitoweo cha nyamapori choma kilichoandaliwa kwa umahiri, akisema kuwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha matumizi ya rasilimali za maliasili kwa njia endelevu.
“Kwa wale ambao wanasema hawajawahi Kula nyamapori choma, nyama hiyo ipo hapa, mishikaki pia ipo na nyama ya kupeleka nyumbani
“Kwahiyo watu wote mnakaribishwa mje kuonja, Kula na kuona
Kweli maliasili ni za kwetu wote” amesema Dkt. Mlay