Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Viti Maalum, Taska Mbogo, amesema Serikali imekuja na mpango mzuri wa Dira ya Maendeleo 2050, unaolenga kuhakikisha Tanzania inafikia hadhi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2050.
Ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akichangia mipango ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Amesema lengo kuu ni kuwa na viwanda vya kutosha vitakavyowezesha uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi.
Ameeleza kuwa ujenzi wa viwanda nchini si jambo jipya, kwani hapo awali kulikuwapo viwanda vingi ikiwemo vya nguo kama Mutex, Mwatex, Urafiki na Kilitex, ambavyo vilitumia malighafi ya pamba inayozalishwa nchini,
Hata hivyo, viwanda hivyo kwa sasa havifanyi kazi kutokana na sera ya ubinafsishaji.
Amesema kuwa wakati huo ubinafsishaji ulikuwa ni lazima, lakini kwa sasa viwanda vingi vilivyobinafsishwa havifanyi kazi.
Ameomba Serikali ivichukue tena ili wakulima waweze kupata soko la uhakika la pamba.
Aidha, amesema kulikuwapo pia viwanda vya kusindika nyama kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, viwanda vya mafuta na jumla ya viwanda takribani 364 vilivyobinafsishwa.
Ameomba Serikali ipitie upya mikataba ya ubinafsishaji ili kuona uwezekano wa kuvirejesha.
Kwa upande wa kilimo, ameishauri Serikali kuwekeza zaidi kwani ndicho uti wa mgongo wa uchumi.
Ameeleza kuwa wakulima wengi hupata hasara kutokana na gharama kubwa za uzalishaji, hususan mbegu na mbolea.
Amehoji kwanini mbegu za mahindi zinazozalishwa sasa haziwezi kupandwa tena, tofauti na mbegu za asili.
Ameomba watafiti wa kilimo wafanye utafiti ili kurejesha mbegu zitakazomsaidia mkulima kujiendesha bila gharama kubwa.
Kuhusu utalii, amesema filamu ya ‘Royal Tour’ imeongeza mapato, hivyo Serikali iendelee kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya hifadhi ili kuvutia watalii wengi zaidi.

