Na Mwandishi Wetu
KATAVI: SERIKALI imetoa Sh. Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa madaraj, vivuko na kufungua barabara inayoanzia Kambanga-Ifinsi mpaka Kijiji cha Bugwe ambapo imewezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mkoa wa Katavi, Japhet Bengesi ameishukuru serikali kwa jitihada hizo.
Amesema fedha hizo zimewezesha kukamilisha ujenzi wa vivuko na daraja la Mto Mnyamasi lenye urefu wa mita 20 pamoja na kufungua barabara ya Kambanga-Ifinsi yenye urefu wa Kilomita 37 inayounganisha vijiji vya Ifinsi, Kambanga na Bugwe vilivyopo kata ya Tongwe Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
“Kikwazo kikubwa kilikuwa katika mto Mnyamasi ambalo ni eneo la bonde hapo awali hakukuwa na mawasiliano lakini kutokana na juhudi za serikali kutuletea fedha, tumeweza kujenga makalavati ya ukubwa tofauti saba na barabara unganishi ambapo imekuwa mkombozi mkubwa maana hili ni eneo kubwa sana la uzalishaji,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mnyamasi, Ngisa Muyanga ametoa shukrani kwa kuwatengenezea barabara hiyo ambayo hapo awali ilipitika kwa shida.
“Tulikuwa tunavuka kwenye maji kipindi cha masika, wakina mama walikuwa wanajifungulia njiani magari yalikuwa hayapiti na tulikuwa tunashindwa kusafirisha biashara zetu, lakini kwa sasa tunaishukuru serikali, watu wanavuka kwa urahisi na magari yanapita katika vipindi vyote,” amesema.
Wakati huo huo Mkazi wa kijiji cha Ifinsi, Ibrahimu Temi amesema, kipindi cha nyuma miundombinu ilikuwa tabu walikuwa wanabeba magunia yenye mazao mabegani kuvuka ng’ambo, lakini sasa magari yanaingia kijijini.