Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeimarisha upitikaji wa miundombinu ya barabara za Wilaya wenye urefu wa kilometa zaidi ya 5000 kwa asilimia 55 kitaifa na asilimia 52 Kimkoa ambapo lengo ni kufikia asilimia 60 ifikapo mwezi Juni, 2025.
Akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), Ismail Mafita amesema hayo katika Semina ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na ongezeko kubwa la bajeti ya Wakala kutoka Sh. Bilioni 25 hadi Sh. Bilioni 52 sawa na ongezeko la asilimia 205.79 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.
Pia amesema mtandao wa barabara za lami katika kipindi hicho umeongezeka kutoka Kilomita 469.47 hadi 636.519, changarawe kutoka Kilomita 1,327.55 hadi 1,686.706 na barabara za udongo zimepungua kutoka Kilomita 3,260.75 hadi Kilomita 2,731.54 kwa mapato ya ndani.
“Katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala tunaendelea kufanya majaribio kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja ya mawe pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha barabara tunazozisimamia.
“Matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya madaraja, huongeza ufanisi, huokoa muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu,” amesema.
Amesema Matumizi ya teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya asilimia 50 ambapo TARURA imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi.
“Hata hivyo Wakala unaendelea na matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi na utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira,” amesema.